Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha

( AUWSA )

MHANDISI IDDY MSUYA AKABIDHIWA RASMI OFISI YA MKURUGENZI AUWSA

Imewekwa: 16 June, 2026
MHANDISI IDDY MSUYA AKABIDHIWA RASMI OFISI YA MKURUGENZI AUWSA

MHANDISI IDDY MSUYA AKABIDHIWA RASMI OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI AUWSA
Kufuatia mabadiliko ya Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji yaliyofanywa na Mheshimiwa Waziri wa Maji, Jumaa Awesso (Mb), tarehe 02 Juni 2026, leo Ijumaa tarehe 12 Juni 2026, Mhandisi Iddy Msuya amekabidhiwa rasmi ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi Justine Rujomba.

Hafla ya makabidhiano imefanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya AUWSA mbele ya Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Bi. Amulikiwa Massawe aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Bodi, na kushuhudiwa na Menejimenti ya AUWSA. Akimkaribisha Mkurugenzi Mtendaji mpya, Bi. Amulikiwa Massawe alimhakikishia ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu yake na kusisitiza kuwa “Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti pamoja na watumishi wa AUWSA watatoa ushirikiano unaohitajika ili kuhakikisha mamlaka inaendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kutoa huduma bora ya maji kwa wananchi.”

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Bodi alitoa shukrani kwa Mhandisi Justine Rujomba kwa mchango wake katika kipindi chote alichohudumu AUWSA na kumtakia mafanikio katika majukumu yake mapya. Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi wa AUWSA, Bi. Amulikiwa Massawe alisema “Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wanakushukuru kwa utendaji wako na wanakutakia kila la heri katika majukumu yako mapya.”

Kwa upande wake, Mhandisi Justine Rujomba akimkaribisha Mkurugenzi Mtendaji mpya alisema:
“AUWSA ina Menejimenti imara na yenye weledi. Mafanikio ambayo mamlaka imeendelea kuyapata yametokana na ushirikiano na kujitoa kwa timu hii. Naomba muendelee kumpa ushirikiano Mhandisi Iddy Msuya kama mlivyonipa mimi katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa AUWSA, Mhandisi Iddy Msuya, aliwashukuru wajumbe wa Bodi na Menejimenti kwa mapokezi hayo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kufanikisha malengo ya taasisi. Akizungumza na Menejimenti alisema “Ili tufikie malengo yetu tunahitaji kufanya kazi kwa ushirikiano. Nawategemea sana katika mawazo, uzoefu na utekelezaji. Sote tupo katika sekta ya maji kwa lengo moja — kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji.”