Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha

( AUWSA )

HUDUMA YA MAJI ISIKWAME: KATIBU TAWALA WILAYA YA ARUSHA AWAKUTANISHA AUWSA, TARURA NA MKANDARASI

Imewekwa: 21 July, 2026
HUDUMA YA MAJI ISIKWAME: KATIBU TAWALA WILAYA YA ARUSHA AWAKUTANISHA AUWSA, TARURA NA MKANDARASI

Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha (DAS), Ndugu Jacob Julius Rombo, ameongoza kikao kilichozikutanisha taasisi mbili za Serikali ambazo ni Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), pamoja na mkandarasi anayetekeleza kazi ya kuhamisha mabomba ya maji katika maeneo yanayojengwa barabara zinazoelekea Uwanja Mpya wa Michezo wa AfCON. Kikao hicho kililenga kujadili namna bora ya kutatua changamoto iliyojitokeza kwa baadhi ya wananchi kukosa huduma ya maji kutokana na kukatwa kwa bomba ya maji katika wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara.

Akizungumza katika kikao hicho, Ndugu Rombo alisisitiza AUWSA na TARURA kuimarisha ushirikiano, mawasiliano na kubadilishana taarifa kwa wakati ili changamoto zinazojitokeza zitatuliwe kwa haraka bila kuathiri upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi, huku utekelezaji wa mradi wa barabara ukiendelea. Alieleza kuwa mradi huo ni wa kimkakati kwa maandalizi ya michuano ya AFCON, hivyo ni muhimu utekelezwe kwa ufanisi na bila ucheleweshaji usio wa lazima. Aidha, Katibu Tawala  huyo aliiagiza TARURA kumsimamia kwa karibu mkandarasi anayetekeleza kazi ya kuhamisha bomba na kumuhimiza kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa AUWSA, Mhandisi Iddy Yazidi Msuya, aliahidi kutoa ushirikiano wa karibu na TARURA katika kuhakikisha changamoto zote zinazojitokeza zinatatuliwa kwa wakati. Alieleza kuwa AUWSA itateua mtumishi maalumu atakayeshirikiana moja kwa moja na TARURA katika kutambua maeneo yote yaliyoathirika, kusimamia uhamishaji wa bomba za maji na kuhakikisha miundombinu yote iliyoathirika inarejeshwa kwa wakati ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji bila usumbufu.