Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha

( AUWSA )

PIC YARIDHISHWA NA UBORESHAJI WA HUDUMA YA MAJI JIJINI ARUSHA

Imewekwa: 14 March, 2024
PIC YARIDHISHWA NA UBORESHAJI WA HUDUMA YA  MAJI JIJINI ARUSHA

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Augustino Vuma (Mb) wametembelea na kukagua Mradi wa kuboresha huduma ya Majisafi na usafi wa mazingira jijini Arusha na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Arumeru uliotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA).

Akizungumza baada ya ukaguzi wa baadhi ya maeneo hayo, Mhe. Vuma  amesema Kamati imeridhishwa na kazi zilizofanyika na kuitaka AUWSA kuitunza na kuitumia vizuri miundombinu hiyo ili iweze kuwahudumia wananchi wa Jiji la Arusha na viunga vyake kwa muda mrefu. 

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AUWSA Mhe. Balozi Daniel Ole Njoolay, amesema AUWSA imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na PIC na itatekeleza Mradi huo kwa lengo la  kuboresha hali ya upatikanaji wa majisafi na uondoaji wa maji taka ili kuboresha afya na hali ya maisha ya wakazi wa Jiji kwa ujumla wake.

Mkurugenzi wa AUWSA Mhandisi Justine Rujomba aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa  kuwezesha utekelezaji wa mradi huu ambao umetatua changamoto za maji Jiji la Arusha na baadhi ya Maeneo ya Wilaya ya Arumeru.

Mradi huo umegharimu jumla ya kiasi cha Shilingi za Kitanzania 520 bilioni ambapo takribani wananchi 1,009,548 wamenufaika na Mradi huo ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa wakazi wanaopata maji kutoka wastani wa watu 325,000 hadi kufikia watu 600,000 wakiwemo wastani wa watu 250,000 wanaoingia na kutoka Jijini kila siku, Wananchi 143,770 kutoka Wilaya ya Arumeru, Wananchi 9,049 Wilaya ya Hai na Wananchi 6,529 kutoka Wilaya ya Simanjiro.