Mwenge wa Uhuru 2024 waweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji Mirerani.
Tarehe 18 Julai 2024.
Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi katika Mradi wa Maji Mirerani unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) kupitia wataalamu wake na kwa kutumia mafundi wa ndani “Force Account”.
Mradi huu uliibuliwa baada Serikali kubaini upungufu wa Maji katika maeneo ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mirerani na kutoa maelekezo kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha kufanya usanifu kwenye visima vilivyochimbwa kupitia Mradi mkubwa wa Maji Jiji la Arusha maeneo ya Valesca na Mbuguni kwa ajili ya kupeleka huduma ya majisafi katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mirerani.
Mradi huo unagharimu jumla ya shillingi bilioni 4.37 fedha kutoka Serikali Kuu na umefikia asilimia 75%, Mradi unazalisha Maji lita Milioni 2.4 kwa siku na utanufaisha wakazi wapatao 57,607 wa maeneo ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mirerani na maeneo ya jirani ya Kata za Shambarai na Naisinyai.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndg. Godfrey Eliakimu Mzava ameipongeza AUWSA kwa kuzingatia na kufuata Sheria na taratibu za manunuzi na malipo kwa kutumia mifumo ya Serikali kama iliyokuwa TANePs na sasa NeST pia amewasisitiza wananchi kutunza Mazingira na Miundombinu ya Maji ili huduma ya maji iwe endelevu.
Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 umeridhia kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huo.