Resources » News and Events

Serikali yatumia Bilioni 514 Kumaliza tatizo la Maji Jijini Arusha

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) imetia saini mkataba na kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering ya nchini China kwa jili ya kuchimba visima kumi na moja (11) eneo la Magereza - Shamba la Mbegu. Visima hivi vitasaidia kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi katika Jiji la Arusha

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Arusha (AUWSA), leo imeingia mikataba ya Dola za Marekani 233,915,581 ambazo ni takribani Shilingi 514,614,278,200 za Tanzania kumaliza kabisa tatizo la maji katika Jiji la Arusha na Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro.
Fedha hizo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambao wamechangia Dola za Marekani 210,962,581 na Serikali ya Tanzania ikichangia Dola 22,953,000 ili kukamilisha mradi huo.

Kazi zitakazotekelezwa ni uchimbaji wa visima virefu, ujenzi wa matenki, ulazaji wa mabomba ya majisafi na majitaka, ujenzi wa mtambo wa kutibu maji, ujenzi wa mabwawa mapya ya kutibu majitaka, ujenzi wa Makao Makuu ya Mamlaka na Ofisi za Kanda pamoja na ununuzi wa vitendea kazi.

Kukamilika kwa mradi huu kutawezesha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wakazi wa Jiji la Arusha kwa asilimia 100 hadi mwaka 2030 na kutapunguza kiasi cha maji yanayopotea kutoka asilimia 45 ya sasa mpaka kufikia asilimia 20. Aidha, mradi utaongeza mtandao wa kuondoa majitaka kwa asilimia 30. Mradi huu unategemea kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda na kuboresha huduma nyingine za kijamii zikiwemo Afya na Elimu.

Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Jiji la Arusha kwa sasa ni asilimia 44, sawa na wastani wa lita milioni 40 kwa siku na mradi huu unategemea kuongeza kiwango na kufikia lita milioni 200 kwa siku.

Download/s File: